Kamati za Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria Bila Malipo Yazinduliwa Simiyu

0


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ameziagiza Kamati za Ushauri wa Kisheria kuhakikisha zinawafikia wananchi hususan walioko vijijini ili waweze kupata haki zao kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Akizungumza  Februari 3, 2026 katika uzinduzi wa Kamati za Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria Bila Malipo uliofanyika katika viwanja vya CCM Bariadi, Mhe. Anamringi Macha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, amesema uwepo wa kamati hizo ni hatua muhimu katika kuimarisha utawala wa Sheria na haki kwa wananchi.

“Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mwananchi anapata haki bila vikwazo. Kamati hizi ni daraja muhimu kati ya wananchi na mifumo ya haki, hasa kwa wale wasio na uwezo wa kugharamia huduma za Kisheria,” alisema Mhe. Macha

Aidha Mhe. Anamringi Macha alisisitiza Kamati za Kisheria kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya Kufanya kazi kwa weledi,uaminifu na bidii.

Vilevile Mhe. Anamringi Macha aliishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa huduma ya kliniki ya sheria bila malipo katika Mkoa wa Simiyu.

“Nimshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Kamati hizi zinazozinduliwa hususan katika Mkoa huu wa Simiyu, kwani kupitia Kamati hizi wananchi watapata huduma za Kisheria zinazowakabili wananchi.” Amesema Mhe. Macha

 Akimwakilisha  Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Bi. Neema Ringo Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria, amesema uzinduzi wa kamati hizo ni utekelezaji wa sera na mikakati ya Serikali ya kuhakikisha huduma ya Kisheria inapatikana kwa wote bila ubaguzi.

“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kushirikiana na mikoa na halmashauri kuhakikisha kamati hizi zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwa ufanisi mkubwa,” amesema Bi. Neema Ringo

Kwa upande wake, Bi. Prisca Kayombo Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu amesema kuanzishwa kwa kamati hizo kutasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika jamii, kwani wananchi watapata ushauri wa kitaalamu kabla ya migogoro yao kufikia hatua kubwa.

“Migogoro mingi ya ardhi, ndoa, mirathi na ajira imekuwa ikiongezeka kutokana na ukosefu wa elimu ya kisheria. Kliniki hizi zitatoa msaada wa moja kwa moja na kuleta suluhu za mapema,” amesema Bi. Prisca Kayombo.

Halfa ya Uzinduzi  ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wanasheria, wadau wa haki, pamoja na wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu, ambapo kliniki ya sheria bila malipo ilianza kutoa huduma mara moja kwa wananchi waliohudhuria, na Kliniki ya Sheria bila malipo inafanyika katika viwanja vya CCM Bariadi Simiyu  hadi tarehe 8 Februari, 2026.

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top