Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 10 Disemba, 2025 ameipokea timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na taasisi zake waliopo katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya kufanya uhamasishaji wa wananchi kuhusiana na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya kilimo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mikutano hiyo.
Mhe. Mtambi amesema wataalamu hao wanapita katika Wilaya tano za Mkoa wa Mara kuanzia leo tarehe 10-15 Disemba, 2025 kufanya uhamasishaji wa masuala mbalimbali na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kushiriki mikutano hiyo.
“Wataalamu hawa wamekuja wakati muafaka tunapoanza msimu mpya wa kilimo na wao watatoa elimu kuhusiana na fursa mbalimbali zilizopo katika taasisi mbalimbali za Serikali kuhusiana na kilimo” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi ameitaja fursa kubwa waliokuja nayo wataalamu hao ni kuwaelimisha wakulima namna ya kufanya uhakiki wa kutambua mbegu halisi iliyosajiliwa na mamlaka husika ambapo mwananchi atatakiwa kufanya hivyo kwa kutumia simu yake ya mkononi ili kuhakikisha mbegu anayoipanda shambani ni mbegu yenye ubora unaotakiwa.
Mhe. Mtambi ameishukuru Serikali kwa kutoa fursa katika sekta mbalimbali za uzalishajimali na kuwahakikishia wananchi wanaozichangamkia fursa hizo wanapata utajiri wa uhakika katika kilimo, uchimbaji wa madini, ufugaji na kadhalika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Ndugu Samson William Poneja amesema timu ya wataalamu ya uhamasishaji wa Kampeni ya Mali Shambani kutoka Wizara ya Kilimo ipo katika Mkoa wa Mara na itafanya mikutano katika baadhi ya Vijiji kuanzia leo tarehe 10-15 Disemba, 2025.
Ndugu Poneja amesema wataalamu hao watatoa elimu kuhusu fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Wizara ya Kilimo na itazungumza na kujibu hoja za wananchi kuhusiana na masuala mbalimbali na leo inatarajia kuanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Amezitaja Halmashauri nyingine zitakazofikiwa na timu ya wataalamu hao awamu hii ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Ndugu Poneja amesema timu hiyo itafanya uhamasishaji kuhusu mbolea ya ruzuku, fursa ya wakala wa pembejeo kwa wakulima, mbegu bora, uhakiki wa mbegu, huduma za ugani, viwatilifu, taarifa za hali ya hewa na ushauri wa wataalamu kwa wakulima.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Ndugu Lepapa Mollel ameishukuru timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo kwa kupanga kuja kutoa elimu kuhusiana na masuala mbalimbali ya kilimo kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Ndugu Mollel ametolea mfano wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo na namna ya kutambua mbegu bora za mazao itawanufaisha wakulima kwa kuwaongezea tija katika kilimo cha mazao mbalimbali.
“Utoaji wa elimu kwa wakulima utawaletea tija hususan wale watakaofuatilia elimu hiyo na kuufanyia kazi ushauri na maelekezo yatakayotolewa na wataalam” amesema Ndugu Mollel.
Tukio hilo limehudhuriwa na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Chanzo: ofisi ya mkuu wa mkoa





