Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), ameihimiza Benki ya Ushirika (COOP Bank) kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa za ulinzi ili kuhakikisha usalama wa fedha za wanaushirika na wateja wake, sambamba na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika Sekta ya Fedha.
Mhe. Chongolo ametoa wito huo tarehe 15 Desemba 2025 jijini Dodoma, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya fedha kiganjani ijulikanayo kama “CooPesa” iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Sekta ya Fedha na Vyama vya Ushirika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Chongolo amesema matumizi sahihi ya teknolojia za kisasa za ulinzi ni muhimu katika kulinda mifumo ya kibenki dhidi ya uchezewaji, udanganyifu na vitendo vingine vya kihalifu vinavyoweza kusababisha hasara kwa wanachama wa vyama vya ushirika na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ameipongeza Benki ya Ushirika (COOP Bank) kwa kuamua kuweka Makao Makuu yake jijini Dodoma, akisema hatua hiyo itaendelea kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa mkoa huo. Amesisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za benki hiyo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Benki ya Ushirika, Bw. Geofrey Ng’urah, amesema huduma ya CooPesa imelenga kuwafikia wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma rasmi za kibenki, hususan walioko maeneo ya vijijini, huku benki hiyo ikilenga kuwafikia zaidi ya wananchi milioni 10 ifikapo mwaka 2030.
Bw. Ng’urah ameongeza kuwa benki hiyo imejipanga kuhakikisha huduma za kifedha zinakuwa nafuu, salama na rafiki kwa wananchi, jambo litakaloongeza ushiriki wa wananchi katika mfumo rasmi wa kifedha na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Chanzo: wizara ya kilimo


