Wanawake na Wasichana Watajwa Kuathirika Zaidi na Nishati Isiyo Safi ya Kupikia

0


Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa wanawake, wasichana na watoto ni kundi linaloathirika pakubwa na matumizi ya nishati isiyo Safi ya Kupikia ya kuni na mkaa ambapo moshi unaotokana na matumizi ya nishati hizo huwa na gesi zenye sumu pamoja na chembechembe ndogo za vumbi zenye viambato vya sumu ambazo huweza kudhoofisha mfumo wa upumuaji na kusababisha magonjwa mbalimbali kwa binadamu.

Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa ni asilimia 16 tu ya watanzania ndio wanatumia nishati safi ya kupikia, hivyo bado kuna magonjwa yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa ambayo yanasababisha vifo vya zaidi ya watu 33,000 kwa mwaka nchini

Wanawake, wasichana na watoto hasa wa maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na wanaoishi katika mkoa wa Mara wanatajwa kuathirika zaidi na nishati isyosafi ya kupikia kutokana na wanawake na wasichana ndio wahusika wakubwa katika kupikia familia huku baadhi yao wakiwa wanapika huwa aidha wmewabeba watoto mgongoni au watoto wanakua karibu na mama au walezi wao jikoni wakisubiri chakula hali inayopelekea na wao kuathirika na nishati hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) inaeleza kuwa moshi unaotokana na matumizi ya nishati isiyo safi huwa na gesi zenye sumu pamoja na chembechembe ndogo za vumbi zenye viambato vya sumu ambazo huweza kudhoofisha mfumo wa upumuaji na kusababisha magonjwa sugu kama kikohozi, homa ya mapafu, kifua kikuu, pumu na saratani ya mapafu. Vilevile, sumu hizo husababisha kuharibika kwa ujauzito, kujifungua kabla ya wakati au kujifungua watoto wenye matatizo ya kiafya.

Magonjwa mengine yanayohusishwa na sumu hizo ni pamoja na magonjwa ya moyo na macho, shinikizo la damu na kupooza. Waathirika wakubwa wa matatizo haya ya kiafya ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake ambao hutumia muda mwingi jikoni kuandaa chakula. Vilevile, ubebaji wa mizigo mikubwa ya kuni migongoni au vichwani huathiri uti wa mgongo, kichwa na miguu ya wanawake na watoto.

 Athari hizi za kiafya husababisha kuelemewa kwa mifumo ya afya kutokana na magonjwa ambayo yangeweza kuepukika kama nishati safi za kupikia zingetumika. Inakadiriwa kuwa takribani watu 33,024 hufariki kwa Mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa katika makazi.

Mkakati huo pia unaeleza kuwa katika jitihada za kutafuta kuni, wanawake na watoto hukumbwa na matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa kutokana na kwenda kutafuta kuni maeneo ya mbali na makazi ya watu ambayo ni hatarishi. Sambamba na hilo, wanawake wengi hukumbwa na kadhia ya kupigwa na waume zao kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta kuni hivyo kuchelewa kurudi nyumbani, jambo linalohatarisha maisha, ustawi wa ndoa na familia.

Chanzo: Mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024-2034)

✍️Imeandikwa na Emmanuel Chibasa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top