Na Angela Sebastian
Kyerwa: Mgombea ubunge jimbo la Kyerwa Khalid Mussa Nsekela amemuomba mgombea mwenza wa kiti cha Urais kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa chama hicho kitakaposhika dola tena kisaidie kutatua changamoto inayowakabili wananchi wa jimbo hilo ya kukosa vitambulisho vya Taifa(NIDA).
Nsekela ametoa ombi hilo baada ya Dk.Nchimbi kumnadi kwa kuwahakikishia wananchi kuwa mgombea huyo anafaa na na atawaletea maendeleo kisha kumpatia nafasi ya kusalimia maelfu ya wananchi ambao walifulika katika mkutano wa mgombea mwenza uliofanyika leo katika viwanja vya stend ya mabasi Nkwenda wilayani Kyerwa.
Nsekela amewaomba wananchi wa jimbo la Kyerwa itakapofika Oktoba 29 mwaka huu kupiga kura kwa wagombea wa chama cha mapinduzi CCM kupiga kura kwa ajili Rais, wabunge na madiwani.
"Nashukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mama yetu Dkt. Samia amefanya na kutekeleza mengi sisi sote ni mashuhuda pia anaendelea kutuahidi mengi ambayo anakwenda kuyatekeleza naomba ili wananchi hawa wanufaike na fursa hizo kuna jambo moja ambalo naomba msaada wako Dkt. Nchimbi ni Nida"
Amesema wananchi wanakosa huduma za msingi ikiwemo mikopo kwa ajili ya kujiletea maendeleo hivyo hii ni changamoto kubwa katika eneo hili.
Naye mgombea mwenza wa wa kiti cha Urais Balozi Emmanuel Nchimbi amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali itaboresha hospitali ya wilaya ya Kyerwa, vituo vya afya vitano, kujenga shule mpya za sekondari nne, ahile za msingi saba.
Miradi mingine itakayojengwa ni pamoja na visima vipya vya maji kutoka visima 334 hadi 426, kuongeza skimu za umwagiliaji kutoka 15 hadi 17.