Na WAF - Dodoma
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe leo Agosti 19, 2025 amepokea tuzo ya utendaji bora wa Kituo cha Huduma kwa Wateja (Afya Call Centre - 119) iliyotolewa na 'Taasisi ya Global Youth Empowerment' Agosti 12, 2025 katika Maonyesho ya Vijana ya Biashara na Uwekezaji Africa Mashariki, yaliyofanyika Zanzibar.
Tuzo hiyo ameikabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Otilia Gowelle wakati wa kikao na Wakurugenzi pamoja na Wakuu wa Idara baada ya kikao cha majadiliano juu ya uboreshaji wa huduma za afya nchini.
Tuzo hiyo ya umahiri wa utoaji wa huduma za Afya kidijitali kwa ukanda wa Afrika Mashariki imetolewa kwa Wizara ya Afya katika kutambua mchango wa kituo hicho katika kutoa elimu ya Afya, ufuatiliaji wa magonjwa na utoaji wa taarifa sahihi za masuala mbalimbali ya afya kwa umma.