Utambulisho wa Matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi Wazinduliwa Zanzibar

0



Na Mwandishi Wetu, WMTH – Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amezindua rasmi Utambulisho wa Matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi – Zanzibar katika hafla iliyofanyika leo Agosti 16, 2025 kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Zanzibar. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Hemed alisema mfumo huu ulizinduliwa rasmi Februari 8, 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), na tukio hili la leo ni la kutambulisha matumizi yake kwa upande wa Zanzibar kuonesha namna wananchi wanavyoweza kupata huduma mbalimbali zilizopo karibu pamoja na kuanza rasmi kwa utoaji wa barua za utambulisho wa mkazi kwa njia ya kidijitali.

Mhe. Abdulla alifafanua kuwa mfumo huo utaondoa usumbufu wa wananchi kulazimika kwenda kwa Sheha kuchukua barua za utambulisho, kwani sasa kila mwananchi ataweza kuomba barua hiyo popote alipo na Sheha au Katibu wa Sheha ataidhinisha maombi hayo mtandaoni. 

Alisisitiza kuwa hili ni jambo la mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za kidijitali na akasisitiza umuhimu wa kila mwananchi kusajiliwa katika mfumo huo ambao sasa ni daftari la kidijitali la wakazi na makazi. Makamu wa Pili wa Rais pia aliagiza barua zote za utambulisho wa mkazi zitolewe kupitia Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA)

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed, alisema Wizara yake inatambua umuhimu wa Mfumo wa Anwani za Makazi katika kuharakisha na kurahisisha huduma kwa wananchi. Alibainisha kuwa Wizara yake itaendelea kuratibu mfumo huo kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa zoezi hili ni endelevu kutokana na ongezeko la miji, makaazi na miundombinu ya barabara na mitaa.

Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, alisema Serikali imejipanga kuimarisha zaidi mfumo huu kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Alisema Wizara yake itaendelea kujenga uwezo kwa watendaji na masheha, kuwezesha upatikanaji wa vishikwambi kwao pamoja na kuhamasisha wadau wengi zaidi kutumia mfumo huu katika shughuli zao za kila siku, hatua ambayo inalenga kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayoendana na azma ya Taifa ya kuimarisha huduma za kidijitali.

Aidha, Waziri Silaa alieleza kuwa Wizara imeandaa mpango wa miaka miwili kuanzia Februari 8, 2025 wenye lengo la kuhakikisha waratibu na watendaji wote 21,487 wa mikoa na halmashauri za Tanzania Bara na Zanzibar wanapatiwa vishikwambi ili kuimarisha utekelezaji na matumizi ya mfumo huo. Kati ya idadi hiyo, 62 ni wa mikoa, 390 wa halmashauri, 3,956 wa kata, 4,269 wa mitaa, 12,333 wa vijiji, 110 wa wadi na 388 wa shehia.

Waziri huyo alihitimisha kwa kusema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unafanikiwa, kwani mageuzi ya kidijitali ni kichocheo kikuu cha utekelezaji wake. Alisisitiza kuwa kama Wizara zenye dhamana ya Mawasiliano na Teknolojia, ni wajibu wao kuwa mstari wa mbele katika kusukuma utekelezaji wa mageuzi hayo makubwa kwa manufaa ya Taifa.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top