Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kutumia Maonesho ya Kilimo ya Nanenane viwanja vya Nzuguni Dodoma, kama jukwaa muhimu la kutoa elimu ya mazingira kwa vitendo, likiwaelimisha wananchi kuhusu mbinu salama na endelevu katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji.
Elimu ya mazingira inayotolewa inasisitiza matumizi ya mbinu kama kilimo hifadhi, uvuvi usioharibu makazi ya viumbe wa majini, pamoja na ufugaji usiochafua vyanzo vya maji na ardhi.
“Tunafundisha wakulima kutumia mbinu za kuongeza tija bila kuharibu ardhi au kuchangia mmomonyoko wa udongo. Wafugaji pia wanapata maarifa juu ya ufugaji wa kisasa unaozingatia kanuni za kimazingira,” alisema mmoja wa maafisa walioko kwenye banda hilo.
Pamoja na elimu hiyo, NEMC inawakumbusha wananchi kuhusu wajibu wa kutekeleza Sheria ya Mazingira, ikiwa ni pamoja na kuzingatia Tathmini ya Athari kwa Mazingira kabla ya kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo au ufugaji.
Katika upande wa uvuvi, wananchi wanapewa maelezo kuhusu athari za uvuvi haramu na matumizi ya zana hatarishi kwa maisha ya majini, huku wakihimizwa kutumia mbinu salama zinazowezesha uvunaji endelevu wa rasilimali za maji.
Wakazi waliofika kwenye banda hilo wameonesha mwitikio chanya, wengi wakikiri kuwa elimu wanayopata imewafumbua macho kuhusu nafasi yao katika kulinda mazingira wanayoyategemea kwa maisha yao ya kila siku.
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaendelea kuvutia taasisi mbalimbali za umma na binafsi, huku kaulimbiu ikisisitiza uchaguzi wa viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi.