Na Emmanuel Chibasa
Simulizi ya kutoka maumivu ya kuachwa hadi mafanikio: Safari ya Zainabu Ramadhan kutoka Musoma-Mara anayeendesha Excavator
Zainabu Ramadhan msichana mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara, ni mfano wa ujasiri na uthubutu. Anaeleza kuwa baada ya kuachwa na mwenza wake, alipitia changamoto nyingi za kimaisha, lakini aliamua kuzitumia changamoto hizo kama ngazi ya kupanda kuelekea mafanikio.
Akizungumza na Musoma News Hub Zainabu amesema kabla ya kuanza kazi yake ya sasa alikuwa kwenye mahusiano na alibahatika kupata mtoto mmoja. Hata hivyo, maisha yalibadilika ghafla baada ya mwenza wake kumuacha, hali iliyomwacha akiwa na jukumu la kumlea mtoto peke yake.
Akiwa katikati ya maumivu na changamoto za maisha, Zainabu aliamua kuvunja mipaka ya fikra za kijamii na kuingia kwenye kazi ambayo mara nyingi huhusishwa na wanaume – kuendesha mtambo wa kuchimba (excavator). Kwa bidii na kujituma, alijifunza ujuzi huo na kuanza kazi, akilenga sio tu kutimiza ndoto zake binafsi, bali pia kuhakikisha mtoto wake anapata maisha bora na elimu anayostahili.
Hata hivyo, safari yake haikuwa rahisi. Zainabu anasimulia kuwa wakati akitafuta mtu wa kumfundisha kuendesha mtambo huo, alikumbana na kikwazo kikubwa cha rushwa ya ngono. Baadhi ya waliokuwa na ujuzi walimwekea masharti ya kimapenzi ili kumsaidia, jambo lililomvunja moyo na kumfanya karibu akate tamaa. Lakini badala ya kukubali kushindwa, aliamua kupambana tena. Hatimaye, alikutana na mwanamke aliyemsikiliza, kumshauri na hatimaye kumsaidia kujifunza bila masharti, jambo lililomfungulia milango ya safari yake ya mafanikio.
Kwa sasa, Zainabu anafanya kazi na kampuni ya Kilimanjaro Mining Rock Block, inayojihusisha na utengenezaji wa tofali za miamba. Anaendelea kuthibitisha kuwa ndoto zinaweza kufikiwa licha ya changamoto.
Zainabu anasema changamoto alizopitia siyo za kwake pekee, bali ni kielelezo cha hali inayowakumba wasichana na wanawake wengi nchini Tanzania. Wengi hukatishwa tamaa na maumivu ya kuachwa kwenye mahusiano au visa vya rushwa ya ngono wanapotafuta fursa za ajira, hali ambayo huwafanya wajione hawana thamani tena.
Lakini simulizi ya Zainabu inabeba funzo kubwa kwamba mwanamke akiamua, hakuna kazi iliyo ya wanaume pekee. Leo anasimama kama kielelezo cha nguvu mpya na uthubutu, akitoa wito kwa wasichana na wanawake wote kutokata tamaa wanapokutana na changamoto kwenye safari ya maisha na kazi.
“Kuna maisha baada ya kuachwa au kukataliwa kazini. Usikubali kuvunjika moyo. Pambana na ndoto zako kwa sababu unaweza kufanikisha,” anasisitiza Zainabu.