Na Angela Sebastian
Bukoba: Mgombea ubunge jimbo la Bukoba mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mhandisi Johnston Mutasingwa amewaomba wanachama wa chama hicho katika jimbo hilo kufuta makundi na kuungana kwa ajili ya kutafuta kura za kishindo za chama hicho.
Mutasingwa ametoa wito leo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo hilo waliomuunga mkono na kumsindikiza katika ofisi ya tume ya uchaguzi Manispaa ya Bukoba kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Amesema umoja na mshikamano ikiwemo kufuta makundi kwa wanachama wa CCM katika kata ya jimbo hilo vinahitajika ili kuhakikisha chama chama mapinduzi kinapata kura nyingi za wagombea wa ngazi ya udiwani,ubunge na Rais.
Aidha amewashukuru wananchi,viongozi wa chama cha mapinduzi kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa kwa kumuamini na kuona anafaa kuipeperusha bendera kwa tiketi ya CCM ili aweze kugombea ubunge jimbo Bukoba mjini.
Kwa upande wasimamizi wa uchaguzi jimbo la Bukoba mjini Melkion Komba wakati akimkabidhi fomu mgombea huyo amesema tume huru ya uchaguzi inazotaratibu zake ambapo kwanza ni kudhibitisha barua ya uteuzi ya mgombea kutoka katika chama chake.
Pia kumkabidhi nyaraka ambazo zina kitabu kitakacho mpatia mwongozo wa masuala mbalimbali na mwisho kumkabidhi fomu ya kugombea nafasi hiyo ambapo pia anatakiwa kuirejesha tarehe 27 mwezi huu akiwa na wadhamini 25 kwa mujibu wa sheria.