RSA Kuendelea Kushirikiana na Wadau wa Usalama Barabarani

0


Na Mwandishi Wetu -  Dodoma. 

MABALOZI wa Usalama Barabarani (RSA) wamehimizwa kuendelea kujitoa na kushirikiana na wadau wa Usalama Barabarani kuielimisha jamii na madereva juu ya kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima. 

Hayo yamezungumzwa na wadau wa Usalama Barabarani katika Mkutano wa Mwaka wa Mabarozi wa Usalama Barabarani ulifanyika katika ukumbi wa Polisi Jamii Jijini Dodoma. 

Ambapo Chuo cha Ufundi Stadi na Mafunzo ya Ufundi (VETA) kimetajwa kuwa mdau muhimu katika kuimarisha usalama barabarani nchini, kupitia mchango wake mkubwa wa kutoa mafunzo kwa madereva katika vyuo vyake mbalimbali.

Akitoa salamu wakati wa hafla ya mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA, Bwire Ally, amesema VETA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha madereva wanapata umahiri na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni za barabarani.

 "Tuna jumla ya vyuo 80, na hadi kufikia mwisho wa mwaka huu tunatarajia kufikisha vyuo 125. Asilimia kubwa ya vyuo hivi vinatoa mafunzo kwa madereva, hivyo usalama barabarani unategemea sana umahiri wao. Kwa msingi huo, VETA ni mdau mkubwa wa usalama barabarani," amesema Bwire.

Kwa upande mwingine, mwakilishi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ASF Castory Willa, amesema jeshi hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na mabalozi wa usalama barabarani ili kulinda maisha na mali za wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA, DCP Johansen Kahatano, amesema mafanikio ya kampeni za usalama barabarani yanatokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali, akiwemo mabalozi wa usalama.

 “Kuanzia mwaka jana tumeshuhudia mabadiliko chanya. Tulifanya majaribio ya safari za saa 24, na RSA walikuwa vinara wa utekelezaji huo kwa kushirikiana na serikali, LATRA na Jeshi la Polisi. Mafanikio hayo ni ushahidi wa umuhimu wa ushirikiano,” amesema.

Awali akisoma risala ya taasisi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Road Safety Ambassadors (RSA), Augustus Fungo, alieleza mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo ongezeko la wanachama kutoka 38 hadi zaidi ya 300 pamoja na usajili rasmi wa taasisi hiyo.

Amelipongeza Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na wadau wengine kwa ushirikiano wao wa karibu.

Mwenyekiti wa RSA Taifa, Mohamed Mpinga, aliwataka mabalozi wa usalama barabarani kuendelea kujitoa kwa moyo mmoja ili kufanikisha lengo la kupunguza ajali na kuokoa maisha ya Watanzania.

Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillius Wambura, Afisa Mnadhimu wa Kamisheni ya Operesheni na Mafunzo, SACP Abdi Issango, amesema usalama barabarani ni suala la lazima kwa kuwa maisha ya mwanadamu hayawezi kutenganishwa na usafiri.

 "Lengo kuu la usafiri ni kufika salama. Mabalozi mna jukumu kubwa la kupaza sauti, kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu," amesema Issango.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top