👉Kiwanda kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati safi nchini
👉REA kugharamia ununuzi wa mtambo wa RAIS
👉Stamico yapania kusambaza Nishati Safi ya Rafiki Briquettes kila kona
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) leo tarehe 22 Julai, 2025 wamesaini mkataba wenye lengo la kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha nishati mbadala (Mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes) mkoani Geita ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 4.5.
Katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ndogo ya REA, Jijini, Dar es Salaam,REA itatoa jumla ya shilingi bilioni tatu na STAMICO itatoa shilingi bilioni 1.5; kwa mchanganuo huo, REA itagharamia ununuzi wa mtambo wakati STAMICO italipia upatikanaji wa kiwanja, ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji wa mitambo.
Mkataba huo umesainiwa na Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.
Mkataba huo utaifanya STAMICO kuwa na viwanda vikubwa vitano vya kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes; viwanda vingine ambavyo vinaendelea na uzalishaji wa mkaa mbadala vipo wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, Kiwira mkoani Songwe, na viwanda vingine viwili vipo mkoani Dodoma na Tabora ambapo vipo kwenye hatua za mwisho za ukamilishwaji kabla kuanza uzalishaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi, Hassan Saidy, amesema kuwa Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia unafikia asilimia 80 kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2034.
“Katika kufanikisha lengo hilo, Wakala unatekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo uwezeshaji katika kuongeza uzalishaji na usambazaji ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa Watu wa vijijini.”
“Utiaji wa saini wa Mkataba huo kati ya REA na STAMICO ni moja wapo ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wakala ili kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa kuona namna ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati safi kwa Wananchi ili waondokane na matumizi ya nishati zisizo safi na salama," amesema.