Marufuku Hospitali za Umma Kuzuia Miili ya Marehemu Kwa Sababu ya Deni la Gharama za Matibabu

0


Na WAF - Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amezitaka hospitali zote za umma kutekeleza kikamilifu maelekezo yaliyotolewa na Serikali, ikiwemo kuhakikisha huduma inatolewa kwanza bila kigezo cha fedha, na kusisitiza kuwa ni marufuku hospitali kuzuia miili ya marehemu kwa sababu ya deni la gharama za matibabu.

Dkt. Shekalaghe ametoa agizo hilo Julai 29, 2025, wakati wa ziara yake katika hospitali za Rufaa za Mikoa jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa si busara wala utu kwa hospitali ya umma kuzuia huduma kwa mgonjwa au kuzuia mwili wa marehemu kwa sababu ya ukosefu wa fedha, kwani lengo kuu la Serikali ni kutoa huduma, si kukusanya fedha.

“Hakuna mwananchi anayepaswa kunyimwa huduma kwa sababu ya kukosa fedha, hayo si malengo ya Serikali, wajibu wetu kupitia Wizara ya Afya ni kuhakikisha huduma zinatolewa, mwananchi ambaye hana uwezo wa kifedha anapaswa kufuata utaratibu maalum uliowekwa, lakini si kukosa huduma. Atachunguzwa, na akikidhi vigezo vya kutokuwa na uwezo, atasaidiwa,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Aidha, amesisitiza marufuku ya kuzuia miili ya marehemu kwa sababu ya madeni ya hospitali, akizitaka hospitali za umma kufuata muongozo wa Serikali unaowataka Waganga Wafawidhi kuhakikisha miili ya marehemu haizuiwi.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa muongozo kwa hospitali kuwa pale mtu anapofariki dunia, mwili wake usizuiwe. Wapeni mwili ndugu zake ili waende kumzika. Hili Mheshimiwa Waziri amesisitiza hivi karibuni akiwa mkoani Tabora, na ninafahamu hospitali zetu zimeanza kutekeleza maagizo haya. Ninatoa msisitizo tena si vyema, si busara kuzuia mwili kwa sababu ya fedha,” ameongeza Dkt. Shekalaghe.

Pamoja na hayo, Dkt. Shekalaghe amewataka wananchi kufuata maelekezo wanayopewa na wataalam wa afya, kujikinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika, na kuwahi hospitali mara wanapoona mabadiliko katika afya zao ili hatua zichukuliwe mapema.

Chanzo: Wizara ya Afya Tanzania

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top