Wizara ya Afya imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha elimu ya afya kwa umma inawafikia Watanzania wote kupitia mkakati mpya wa kitaifa unaolenga kuboresha ubora, ufanisi na upatikanaji wa taarifa sahihi za kiafya.
Akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuidhinisha rasimu ya Mpango Mkakati wa Elimu ya Afya kwa Umma, Julai 15 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Otilia Gowelle, amewataka wajumbe wa kikao hicho kukamilisha mapema kazi ya kuhuisha rasimu hiyo ili kuruhusu hatua za mwisho za kuidhinisha na kuanza utekelezaji wake kwa haraka.
“Kasi ya utendaji inapaswa kuongezwa na tunahitaji kumaliza hatua hii muhimu ili twende mbele kwa hatua za uidhinishaji rasmi na utekelezaji. Huu mpango ni chombo muhimu cha kuboresha afya ya jamii kupitia maarifa sahihi,” amesema Dkt. Gowelle.
Dkt. Gowelle pia amesisitiza umuhimu wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa, akihimiza utengenezaji wa vielelezo vya kisasa vitakavyosaidia kufikisha elimu ya afya kwa wananchi kwa njia rahisi, shirikishi na yenye ushawishi.
“Mpango huu unajumuisha mifumo madhubuti ya ukusanyaji wa taarifa zitakazowezesha ufuatiliaji wa kina kuhusu jinsi elimu ya afya inavyowafikia wananchi. Hili litasaidia kufanya maamuzi sahihi na ya wakati,” aliongeza.
Kwa upande wake, Dkt. Ona Machangu, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, ameeleza kuwa ushiriki wa wadau wengi katika mchakato huu ni uthibitisho wa imani kubwa waliyonayo kwa kazi ya Wizara ya Afya.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa rasimu hiyo kutatoa dira mpya ya ubora na thamani katika utoaji wa elimu ya afya.
“Tunapoongeza wigo wa teknolojia, tunajiandaa kuleta mapinduzi ya kweli katika elimu ya afya kwa kutumia majukwaa ya kidijitali, mitandao ya kijamii, programu za simu, na mifumo mingine ya kisasa inayofikika kwa wananchi wengi zaidi,” amesema Dkt. Machangu.