HAIPPA PLC Yazindua Kampeni ya Smatika Kuhamasisha Uwekezaji Kwa Watanzania Milioni 20

0


MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya Umma ya HAIPPA PLC, Boniphace Ndengo, amesema kuwa kampuni hiyo imejidhatiti kikamilifu ili ifikapo mwaka 2030 iwe imewafikia Watanzania takribani milioni 20 ili waweze kufahamu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uwekezaji.

Kampuni hiyo yenye makao Makuu yake Mjini Musoma, inajishughulisha na utoaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na masoko,mitaji, ushauri wa kibiashara, urasimishaji, uendelezaji wa biashara, kukuza ubunifu, ujenzi wa Makampuni ya Umma na uwekezaji.

Akizungumza mwishoni mwa wiki mjini  Musoma, Ndengo amesema kuwa katika kufanikisha malengo hayo, HAIPPA PLC imezindua kampeni maalum endelevu kuanzia Julai Mosi, 2025, ijulikanayo kama "Smatika na HAIPPA PLC."

Alieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuwafikia Watanzania wa makundi yote wakiwemo vijana, wazee, wanafunzi, watoto, watumishi, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wajasiriamali, na wavuvi.

Ndengo alibainisha kuwa kampuni hiyo ilianzishwa Oktoba 27, 2022 na wanahisa waanzilishi wanane, wakiwa na mtaji wa Shilingi milioni 3. Ambapo kwa sasa  idadi ya Wanahisa ni 546, Mtaji wa hisa hadi mwezi Juni 30, 2025 ni hisa 444,000, zenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Milioni 222.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa Kampuni hiyo,  ililikuwa ni kuwa akademi bora ya uwekezaji Afrika, huku dhamira ikiwa ni kubuni, kujenga, na kuwekeza kwenye miradi mikubwa barani Afrika. Kwa sasa kampuni hiyo inaendelea kukua, imefungua ofisi katika mikoa mbalimbali hapa nchini na inaendelea kutoa huduma kidigitali.

Aidha, amesema kuwa jukumu jingine kubwa  la  HAIPPA PLC ni kuwezesha umma kushiriki katika miradi mikubwa ya uwekezaji kupitia kampuni za umma na ubia kati ya serikali na sekta binafsi.

"Mwezi huu wa Julai, 2025 tumetimiza siku 1,000 tangu kuanzishwa kwa HAIPPA PLC. Tumeona tuzindue kampeni mpya itakayotupeleka katika viwango vya juu zaidi. Tanzania ina watu wazima takribani milioni 40, lakini ni asilimia 0.5 pekee ya watu hao ndiyo wanashiriki katika uwekezaji mkubwa kama vile umiliki wa hisa kwenye makampuni ya hisa. Hii inamaanisha ni watu takribani 200,000 tu kati ya milioni 40," alisema Ndengo.

Ameongeza kuwa HAIPPA PLC kama kampuni mpya ya uwekezaji imekuja na mkakati mahususi ambao unakusudia kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, angalau Watanzania milioni 20 wawe wanajua na wanashiriki katika fursa za uwekezaji, akisema kuwa huu ndio mfumo unaotumika duniani kote.

Akitolea mfano wa kimataifa, amesema Marekani ina asilimia 60 ya watu wazima wanaoshiriki katika uwekezaji, Singapore asilimia 48, Korea Kusini asilimia 40, China asilimia 24, na India asilimia 17, huku Tanzania ikiwa na asilimia 0.5 tu. Ndengo alisema hali hiyo inasababisha fursa nyingi za uwekezaji mkubwa, kama madini, nishati, miundombinu na kilimo, kubebwa na makampuni kutoka nje ya nchi.

"Makampuni haya yanakuja hapa kama ya kigeni, lakini nyumbani kwao ni kampuni za hisa zenye wanahisa 40,000 hadi 100,000 ambao wanashiriki kujenga mitaji. Wanawapa menejimenti zao zije kufanya biashara barani Afrika. Elimu wanayosoma kule kwao ipo pia hapa Tanzania, sisi wasomi na wataalam wa uchumi na biashara tunaweza kuwawezesha Watanzania kushiriki kwenye uwekezaji mkubwa wa namna hiyo," alisema Ndengo.

Ndengo, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), alisisitiza umuhimu wa kuunda kampuni za umma zitakazowawezesha Watanzania kushiriki katika uwekezaji mkubwa kwa kupitia umiliki wa hisa.

Amesema HAIPPA PLC kama kampuni ya umma imeanzishwa kwa lengo la kuwashirikisha Watanzania kwenye fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali za kimkakati kama kilimo, madini, biashara, ujenzi na nishati. Watanzania wanahimizwa kumiliki hisa za kampuni hiyo ili ziwape fursa kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Ndengo alibainisha kuwa kwa sasa kampuni hiyo imeanza na sekta ya masoko kwa kuwasaidia wazalishaji wa bidhaa nchini kuuza katika masoko makubwa kwa faida zaidi. Mkulima anayeshirikiana na kampuni hiyo anapata faida mara mbili ya kwanza kwa kuuza mazao kwa HAIPPA PLC, na ya pili kwa kupata gawio la faida kama mwanahisa.

"Kampeni yetu 'Smatika Kiuchumi na HAIPPA PLC' inaleta fursa tatu kuu. Fursa ya kwanza ni kuhakikisha kila Mtanzania anamiliki hisa 1,000 za kampuni hii. Hisa hizi zinaweza kununuliwa kidogo kidogo ndani ya miezi 12. Ukifikia hisa 1,000 unakuwa mwanahisa mwenye haki ya kushiriki fursa zote za kimkakati nchini kama kilimo, nishati, miundombinu na utalii," alisema.

Aidha, amesema kampeni hiyo inaambatana na mpango wa "Tumia Tukurejeshee Kikubwa" ambapo matumizi ya huduma au bidhaa zinazohusiana na HAIPPA PLC yatarudishiwa sehemu ya thamani kwa wanachama wake. Mfano, wazazi waliowapeleka watoto kwenye shule zinazoshirikiana na HAIPPA PLC watapokea marejesho ya sehemu ya ada au mapato yanayorudi kwa mwanachama.

Amesema mpango huo utaanza na makundi ya wakulima kwa kununua pembejeo na vifaa kupitia mifumo ya HAIPPA PLC na baadaye utaenea katika sekta nyingine kama nishati, ambapo wale wanaonunua petroli kupitia mifumo ya HAIPPA nao watanufaika.

Hatua hiyo inalenga kuchochea mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na taifa. Fedha zitakuwa zikizunguka kutoka kwa mwananchi kwenda HAIPPA PLC na kurudi kwa mwananchi kwa njia ya gawio au marejesho ya matumizi.

Kuhusu faida ya hisa, amesema mtu anayemiliki hisa 1,000 anaweza kupata gawio la Shilingi 50,000 kwa mwezi kutoka HAIPPA PLC, hali inayompa kipato cha ziada huku akiendelea na shughuli zake nyingine.

Aidha, alibainisha kuwa hisa ni mali ya kudumu na itakuwa kitegauchumi hata baada ya mmiliki kufariki, hivyo watoto na wajukuu wanaweza kunufaika.

"Niwaombe Watanzania kutoka maeneo mbalimbali wachangamkie fursa hii kwa ajili ya maendeleo yao. "Tunatambua kuwa hisa zina tabia ya kukua thamani. Tunakadiria kuwa ifikapo 2030, hisa ya HAIPPA PLC itauzwa kati ya Shilingi 5,000 hadi 7,500, wakati sasa inauzwa Shilingi 1,000. Usipitwe na fursa kwa uzembe," alisisitiza.

SERIKALI YAPONGEZA MWELEKEO WA HAIPPA PLC.

Katika Mkutano Mkuu Maalum wa utambulisho wa huduma za HAIPPA PLC uliofanyika Januari 30, 2025 katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mjini Musoma (MCC), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (aliyewakilishwa na Gambales Timotheo  Mkuu wa Idara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara) aliipongeza kampuni hiyo kwa kusaidia kusukuma ajenda ya maendeleo.

Kupitia hotuba yake, Kanali Mtambi aliwataka wananchi na makundi yote kuchangamkia fursa zinazotolewa na HAIPPA PLC huku akiitaka kampuni hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili watambue umuhimu wa uwekezaji na kutumia soko la hisa la kampuni hiyo kwa maendeleo yao.

Alibainisha kuwa,  Serikali ya Mkoa huo iko tayari kushirikiana na wadau wote wa maendeleo akiwemo HAIPPA PLC kukuza uchumi wa wananchi na Mkoa kwa ujumla. Na Wananchi waendelee kuwa mabalozi wa kuitangaza vyema Kampuni hiyo na huduma zake zichochee Kasi ya ukuaji wa uchumi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top