Na Hamida Ramadhan- Dodoma
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema Miradi yoyote tunayoisimamia ikiwa ina harufu ya rushwa, haitaweza kufika mwisho.
Akizungumza leo katika banda la Kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Mhe. Kihenzile amesema kuwa rushwa katika miradi ya maendeleo si tu inachelewesha utekelezaji bali inakatisha matumaini ya wananchi.
"Kama tunavyojua mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, matarajio yetu na mahitaji yetu TAKUKURU kutusimamia vyema ili nchi ipate viongozi waadilifu na wa kizalendo,” amesema Mhe. Kihenzile kwa msisitizo.
Aidha amesema Serikali imejipanga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kuhakikisha kuwa miradi ya uchukuzi inatekelezwa kwa viwango vya juu na kwa manufaa ya wananchi, huku akibainisha kuwa mafanikio ya sekta hiyo yanategemea usimamizi thabiti usioyumba mbele ya mianya ya rushwa.
"Niitake Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wadau wa usimamizi wa miradi kuhakikisha fedha za umma zinalindwa kwa nguvu zote, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa viongozi kusikiliza kero za wananchi, kutoa elimu ya sera na kufikisha ujumbe wa uwajibikaji kwa taasisi za Serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uelimishaji Umma -TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Faustine Malecha amesema
Wataendelea kutumia jukwaa la Wiki ya Utumishi wa Umma kutoa elimu kuhusu rushwa katika maeneo mbalimbali, na kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi kwa uadilifu na bila kushawishiwa kwa rushwa.
“TAKUKURU tumekuja hapa kutoa elimu kuhusu madhara ya kutoa na kupokea rushwa tunawaelimisha wananchi ili kuhakikisha kwamba hawachagui viongozi wanaonunua nafasi kwa kutoa rushwa kwa sababu viongozi wa aina hiyo hawawezi kuwaletea maendeleo,” amesema