Na Emmanuel Chibasa
Binti ni mtoto
Sio mke, hii ni kauli mbiu ya mwaka 2025 ya Jukwaa la Mtandao wa Kutokomeza ndoa
za Utotoni nchini Tanzania katika mapambano dhidi ya ndoa za utotoni na vitendo
vya ukatili nchini Tanzania
Licha ya
kauli mbiu ya binti ni mtoto sio mke Kuhimiza mabadiriko ya Sheria ya ndoa ya
mwaka 1971, lakini bado zipo baadhi ya mila na desturi zilizopitwa na wakati zinaendelea
kuwaathiri wasichana na wanawake hapa nchini.
Fuatana nami
katika makala hii ya simulizi za mabinti walio na umri chini ya miaka 18 kutoka
katika mkoa wa Mara, ambao wanaishi katika kituo cha nyumba salama Iliyopo Kyabakari Katika wilaya ya Butiama mkoani Mara, baada ya kukimbia familia zao kutokana na kulazimishwa kukeketwa na kutolewa huku wakiwa Watoto ambao hawajafikisha umri wa miaka 18, wakieleza magumu waliyopitia na
wito wao kwa wazazi,walezi, Jamii na Viongozi kwa ujumla.
Ripoti ya utafiti ya afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, Inaonesha kuwa Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa mitano hapa nchini, inayoongoza kwa mimba za utotoni ambapo mkoa wa Songwe ndio unaongoza kwa kuwa na asilimia 45%, ukifuatiwa na mkoa wa Ruvuma wenye asilimia 37% Katavi ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 34%, Mkoa wa Mara ukishika nafasi ya nne ukiwa na asilimia 31% huku mkoa wa Rukwa ukishika nafasi ya tano ukiwa na asilimia 30%
![]() |
Ripoti nyingine ya
utafiti ya mwaka 2024 pia inaonesha mkoa wa Mara, unashika nafasi ya tatu kwa
matukio ya ukatili wa kijinsia kwa kuwa na asilimia 28, huku mikoa ya Arusha na
Manyara ikiwa vinara wa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa kuwa na asilimia 43%
Hali hii
inadaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya mila na desturi kandamizi
zilizopitwa na wakati.
Mila hizi zinaendeleza mfumo dume kwa wazazi na walezi hususani wanaume kulazimisha mabinti kuolewa kwa lengo la kujipatia mali na fedha bila kujali maamuzi ya Binti husika au mama mazazi wa binti kusikilizwa wakati wa Kufanya maamuzi, jambo linalowaweka hatarini wasichana katika vitendo vya ukatili wa kijinsia, hali inayopelekea baadhi hulazimika kukimbilia kwenye nyumba salama zilizopo katika wilaya za Butiama, Serengeti na Tarime na Musoma ili kutafuta hifadhi, usalama na msaada wa kisaikolojia katika masharika yanayotoa huduma hiyo.
Mabinti hawa
wanaokimbia familia zao kutokana na ndoa za utotoni na uwekezaji, wanakua
wanapitia changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutosikilizwa na kutokua na uhuru
wa kufanya maamuzi na simulizi za maisha za maisha wanayopitia zinaweza
kusaidia kuleta mabadiriko katika jamii kutokana na visa na mikasa
wanavyokumbana navyo hadi kufanikiwa kukimbia familia zao na kwenda Kwa ndugu, jamaa au marafiki pamoja na kufika katika vituo vya nyumba salama
kutafuta hifadhi.
Hivi umewahi kufikiria mzazi anaweza kumlazimisha binti yake kuolewa ili apate ng'ombe ambazo zinatakiwa kutumika kwa mdogo wake ambaye pia yuko chini ya miaka 18 ili pia akatoe mahali ili apate mke? Basi hiki ni kisa kimoja wapi tu Kati ya visa vingi walivyonavyo mabinti wanaoishi nyumba Salama Butiama.
Ni saa kumi
na mbili na dakika hamsini jioni nafika hapa katika kijiji cha Kyabakari kilichopo
katika wilaya ya Butiama mkoani Mara, ambapo inapatikana ofisi na kituo cha
nyumba salama cha Hope For Girls and Women Tanzania, Kituo kwa ajili ya
kuhifadhi wasichana waliokimbia kutoka katika familia zao ili kuepukana na ndoa
za utotoni pamoja na ukeketaji kutoka Butiama na maeneo mengine ya mkoa wa
Mara.
Baadhi za wilaya katika mkoa wa Mara bado zinaonekana kuwa nyuma katika swala zima la mila na desturi ambazo zinaonekana kumkandamiza
msichana na mwanamke ambapo ndoa za utotoni ni moja ya mila ambazo inaonekana
kuhalalishwa na jamii ya kikurya.
Wegesa
Nyamuhanga (Sio Jina lake halisi) Mwenye umri wa miaka 18 mkazi wa kijiji cha Kinyambwiga wilaya ya Bunda Mkoani Mara, ni kati ya
wasichana wanaodaiwa kuolewa akiwa bado
na umri mdogo wakati anaishi na wazazi
wake huko katika kijiji cha Kinyambwiga.
Anasema mwaka 2020, aliolewa akiwa na umri wa miaka 15 , Alilazimishwa kuolewa na Mama
yake mzazi baada ya baba yake mazazi kufariki
kwa mahali ya ngombe 6 na kijana mwenye umri wa miaka 18.
Anasema wazazi upande wa mume walipoenda kumchumbia kwao, akakataa lakini mama yake mzazi alimlazimisha akaenda kuolewa, lakini ndoa ilimshinda akakimbia na akamaliza mwezi mzima huko alipokimbilia lakini badae walipata taarifa nilipo wakaenda kumfuata, wakaenda ofisi ya kijiji kuendesha kesi ambapo maamuzi yalitolewa ng”ombe warudishwe sababu alikataa kurud kwenye ndoa.
“Nilirudi
kuishi nyumbani lakini mama aliendelea kunilazimisha kurudi huko nilipokua
nimeolewa sababu yeye hawezi kurudisha ng’ombe, Nilivyoona mama anaendelea
kunilazimisha kurudi na maisha yakawa magumu nikaona bora nitoroke nikaja hapa
Butiama nikakutana na mchungaji Johanes akanipelekea kituo cha usalama jirani
na mahakama wakamuita mzazi wangu lakini mimi nilikataa sirudi nyumbani ndio
wakanileta hapa nyumba salama
Nilipoingia
kwenye ndoa, mwanaume alikua ananipiga kila siku ananilazimisha niende shambani
lakini yeye aendi, ananigombeza kila siku akawa ananichonganisha na wazazi wake
anasema na tabia mbaya, mara siwajali wazazi wake kwenye chakula, nilivyoaona
mateso yamezidi nikaondoka kurudi nyumbani lakini nilipofika huko mama nae
akawa ananipiga ananilazimisha kurudi.
Nawashauri wazazi wasipende kuwalazimisha watoto wadogo uolewa, waache wafikishe umri mkubwa, waache kwanza watoto wasome na kutulia na familia zao” Amesema Wegesa
Kwa wasichana
wadogo, hali hizi hufanyika kupitia shinikizo kutoka kwa familia, hasa kwa baba
ambaye mara nyingi hutumia nafasi yake kama kichwa cha familia kuwalazimisha
mabinti kuolewa kwa lengo la kupata mali – hasa ng’ombe kwa ajili ya matumizi
ya familia.
Katika jamii
nyingi zenye mfumo dume, maamuzi yote ya familia hufanywa na baba, huku mama na
binti husika wakinyimwa haki ya kutoa maoni au kupinga maamuzi hayo. Hali hii
huwanyima wasichana haki ya kupata elimu, huathiri afya yao ya mwili na akili,
na kuwaweka katika mzunguko wa umasikini na utegemezi wa maisha yote.
Veronica Ryoba(sio
jina lake halisi) anasema pia mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 13 baba yake
mzazi alimlazimisha kukeketwa ili aweze kupata mahali na mahali itakayopatikana
iweze kumsaidia mdogo wake wa kiume aache kusoma ili aweze kutumia mahali hiyo kuoa.
Amesema baada
ya baba yake kumuua mama yake kwa panga baada ya kurudi nyumbani na kukuta
hajaachiwa chakula na baada ya tukio hilo ndipo aliamua kutoroka nyumbani baada
ya kuona msada aliokua anaupata kwa mama yake haupati tena huku baba akiendelea kumlazimisha kukeketwa
ili aolewe.
“Mwaka 2020
nilikimbia ukeketaji kwa sababu baba yangu alikuaga mlevi sana na alikua
anataka mimi nikeketwe ili niolewe apata mahali ambayo alitaka imsaidie mdogo
wangu wa kiume aache kusoma naye aweze kuoa na kuendelea na maisha yake
Kutokana baba
kuwa mlevi siku moja mama alikua hana hela ya kununua mboga baba aliporudi
akiwa amelewa akamuomba mama chakula, mama akamwambia hakuna na hela ya kununu
chakula ndipo baba akachukua panga na kumkata mama hadi akafariki.
Baada ya kifo
cha mama niliamua kutoroka nyumbani kutokana na kukosa mtetezi ambaye alikua
anatetea ni nisikeketwe na nikakimbilia kwa baba mdogo ambaye alinizaidia
kunisomesha kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na baada ya kuhitimu ndio
nikakimbilia katika kituo hiki cha nyumba salama Butiama.
Nilipofika
hapa nyumba salama nilipokelewa vizuri nikawaeleza changamoto nilizopitia kule
kijijini, wakanisaidia kuniendeleza kielemu kuanzia kidato cha kwanza hadi
nimehitimu mwaka jana kidato cha nne shule ya sekondari Kyabakari na nimefaulu
na nategemea kuendelea na masomo yangu.” Anasema Veronica
Ameongeza
kuwa ukatili aliofanyiwa umeathiri pakubwa maisha yake kwanza kama mzazi wake
angefanikiwa kumkeketa asiwengeza kufikia malengo yake ya kumaliza elimu ya
msingi na sekondari.
Kwa upande wake anatoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwa watetezi wa watoto wa kike maana huko maeneo ya vijijini wanaamini kuwa watoto wa kike hawawezi kuwasaidia wazazi wao na hawawezi kusoma na wanaamini kwamba mtoto wa kike akiwa amehitimu darasa la saba inatakiwa akeketwe ili aozeshwe ili awape mahali jambo ambao sio sahihi kwani nao wanahitaji kufikia malengo na kutimiza ndoto zao
Wakati Wegesa
Nyamuhanga na Veronica Ryoba wakilazimishwa kuolewa na wazazi wao lakini hali
ni tofauti kwa Lucia Wambura (Sio jina lake halisi) ambaye anaeleza kuwa baba yake mzazi alifariki
mwaka 2020 na alikua hataki watoto wake wakeketwe lakini baada ya baba yake
kufariki ndugu wa baba yake walitaka akeketwe mara baada ya kumaliza mtihani wa
darasa la saba.
“Mimi kwa
historia yangu nyumbani baba yetu alikua anapinga hii mila ya ukeketaji na
alikua anakinzana na ndugu zake wote, sababu walikua wanafanya vitendo hivyo kwa
familia zao, Kwa bahati mbaya baba yangu mwaka 2020 alifariki nikiwa
darasa la tatu na baada ya hapo nilianza kufatiliwa na ndugu upande wa baba ili
nikakeketwe.
Yani nilikua
nataka kukeketwa mara baada ya kumaliza mtihani wa darasa la saba ila sikutaka
ndipo nilipokimbia nyumbani na kukimbilia kwao na rafiki yangu ambaye
tumemaliza nae darasa la saba ambapo mama yake alinipeleka dawati ambao ndio
waliwailiana na huku nyumba salama ambao walinichukua na mpaka sasa naishi
hapa.
Kibinafsi ni
vigumu sana kutokuishi na familia yako na mimi nilizoea na nilijua siku zote
ntaishi na familia yangu ila kwa sasa nipo huku nyumba salama naishi na mabinti
wenzangu, Kuondoka nyumbani pia kuliathiri masomo yangu maana muda mwingine
nikikaa nasoma nawaza nyumbani, nawaza kule nyumbani wanafanyaje na sio tu
masomo bali hata maisha yangu ninapokaa huwa najiuliza kuhusu familia yangu na
ndugu zangu wengine niliowaacha kule nyumbani.
Naishauri jamii inayoendeleza mila ya ukeketaji iachane nayo, kwa sababu inatuathiri sisi mabinti kisaikolojia na kuacha na imani potofu kuwa binti asiyekeketwa hawezi kuolewa na mwanaume ambaye sio wa kikurya hali inayomfanya binti kufikiria ni nani atakaemuoa na maisha yake ya baadae yatakuaje” Amesema Lucia.
Katika jamii
ya Kikurya, mila ya ukeketaji imeendelea kuwa kichocheo kikuu cha ndoa za
utotoni. Wasichana wengi hulazimishwa kufanyiwa ukeketaji wakiwa na umri mdogo,
kwa madai kwamba ni njia ya kuwaandaa kutoka hatua ya utoto na kuingia kwenye
utu uzima, ili wawe tayari kuolewa.
Mila hii
huwasilishwa kwao kama jambo la heshima na utambulisho wa kijinsia, lakini kwa
undani wake, ni mfumo wa ukandamizaji unaonyima wasichana haki ya kufanya
maamuzi kuhusu miili yao na maisha yao ya baadaye. Baada ya kukeketwa,
wasichana huchukuliwa kuwa tayari kuolewa, hata kama bado ni watoto kiumri na
kiakili.
Wengi wao
hulazimishwa kuolewa na wanaume wazee kwa lengo la familia kunufaika kwa
mahari, jambo linalowatupa nje ya mfumo wa elimu na kuwaweka kwenye hatari
kubwa ya madhara ya kiafya, mimba za utotoni, na ukatili wa kijinsia. Mfumo
huu, unaoendeshwa na imani potofu na utawala wa mfumo dume, huwakosesha
wasichana fursa ya kujiendeleza na kujenga maisha bora.
Ndoa za
utotoni katika jamii ya Kikurya, msichana ambaye hajafanyiwa ukeketaji
huchukuliwa kuwa bado na hafai kuolewa,
Kwa mila na desturi hizo, ukeketaji huonekana kama kipimo cha ukomavu wa
msichana na hatua ya lazima kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Rhobi Samwelly na Mkurugenzi wa shirika la Hope For Girls and Women Tanzania na Kituo cha
Nyumba Salama Buatiama, anasema licha ya vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike
kupungua katika mkoa wa Mara lakini bado tatizo na mfumo dume na mila
zilizopitwa na wakati viachangia tatizo hilo kuendelea kuwepo na wasichana
kukimbia familia zao na kutafuta hifadhi katika nyumba salama.
Amesema kwa
sasa hali ya vitendo vya ukeketaji kwa mkoa wa Mara vimepungua ikilinganishwa
na miaka ya nyuma na nyumba salama za Butiama na Serengeti zimekua zikipokea
mabinti wengi inapofika msimu wa ukeketaji lakini tatizo la mfumo dume bado
linaonekana kikwazo kwa wasichana.
“Kwa mfano msimu wa ukeketaji uliokwisha ukiacha wa mwaka jana tuliweza kupokea watoto 480 na idadi hii ilikua ni kubwa na huko nyuma tumekua tukipokea hivyo hivyo lakini katika msimu wa ukeketaji wa 2024 nyumba zetu salama zote mbili tuliokea watoto 347" Amesema Rhobi
"Hali ya mfumo
dume kwa kweli inachangia kuendelea kuwepo kwa ndoa za utotoni na mila na
desturi kandamizi, kwa sababu mara nyingi katika jamii yetu baba wanasema ndio
wasemaji wa mwisho na wao ndio wenye kufanya maamuzi na mwanamke hana nafasi ya
kuzungumza.
Kwa mfano
pale ambapo baba anapoamua binti kuolewa mara nyingi akina mama wanashindwa
kuzuia maamuzi hayo maana wanamsikiliza baba akiishamaua hakuna wakupinga
maamuzi yake, hali hii pia inasababishwa na mama kutokua na uchumi na kuwa
tegemezi kwa baba.
Katika kuwapa elimu na kuwajengea uwezo wanawake na kuchukua hatua za kujishughulisha kiuchumi mara nyingi huwa wanawaeleza na kuuliza waume zao kwamba kwanini huyu binti yetu aolewe na asisome na wamekua wakikataa na kupinga ndoa hizo na kueleza kama ni mali basi mama atachangia kufanikisha jambo hilo hata kama ununuzi wa ng’ombe ili tu binti aendelee na masomo” Amesema Rhobi.
Baada ya
kufanya mahojiano na Rhobi Samwelly, Mkurugenzi wa shirika la Hope For Girls
and Women in Tanzania, ambaye alieleza kwa kina kuhusu tatizo la ndoa za
utotoni na mchango wa vituo vya nyumba salama katika kusaidia wasichana
wanaokimbia ukatili, nilibaki na maswali ya kujiuliza Je, ndoa hizi za utotoni
zinatambulika kidini? Na je, dini inasemaje kuhusu ndoa?
Nimepata
nafasi ya kuzungumza na kiongozi wa dini Sheikh Omari Ali Khamisi kutoka Masid Zanzibar Musoma, anasema ndoa kwa mujibu wa dini ya kiislamu na kwa mujibu wa sheria za
dini , ndoa ni ibada na mtu anapoingia kwenye ndoa ameingia kwenye taasisi ya
ibada na inaongozwa kwa kanuni zake.
Amesema mtu
anaingia katika kanuni hizo anakua na mwenza wake, wakaafikiana na kushauriana
kufuata kanuni kwa mujibu wa sheria ya kiislam wanakua wameingia kwenye ndoa.
“Tunapozungumzia
ndoa za utotoni, tunazungumzia ndoa ambazo ziko chini ya ule umri ambao
unatambulika kisheria ima kitamaduni, au sheria ya nchi au kwa madhehebu na
imani tofauti tofauti.
Kwa mfano kwa
mujibu wa sheria umri unaoruhusiwa mtu kuingia kwenye ndoa awe na umri za ya
miaka 18 na kuendelea lakini ndoa hizi za utotoni ni pale athari za umri
unapoonekana ambapo binti anakua hana fikra ya moja ya kujitegemea, hana uchumi
wa moja kwa moja wa kujitegemea, anafanyiwa maamuzi na watu wengine,
anaendeshewa uchumi na watu wengine.
Ili
kutokomeza tatizo hili kwanza inapaswa kutolewa elimu baina ya mtu na mtu,
familia, kitongoji, kijiji na maeneo mbalimbali katika jamii kuelimishana madhara
yanayopatikana kuhusiana na ndoa za utotoni, madhara ya kiafya yanayopatikana
na ukeketaji na ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Tarehe 9
June, 2025 Waziri wa maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum,
Mhe. Dkt Dorothy Gwajima Akitangaza Matokeo ya utafiti wa kitaifa wa ukatili
dhidi ya watoto na Vijana ya mwaka 2024.
Alisema Matokeo ya utafiti wa Machi-Juni, 2024 yanaonesha ukatili umeshuka kwa kiwango kikubwa ukilinganisha utafiti wa 2009 ambapo,Kwa Watoto wa kike Ukatili wa kingono umepungua kutoka 33% hadi 11%; Ukatili wa kimwili umepungua kutoka 76% hadi 24%; na Ukatili wa kihisia umepungua kutoka 25% hadi 22%.
Kwa watoto wa kiume: Ukatili wa kingono umepungua kutoka 21% hadi 5%; Ukatili wa kimwili umepungua kutoka 74% hadi 21% na Ukatili wa kihisia umepungua kutoka 31% hadi 16%. Na walengwa ni watoto 11,414 wenye umri wa miaka 13 hadi 24 kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Ndoa na mimba za utotoni ni aina za ukatili wa
kijinsia kwa wasichana huathiri maisha yao kwa kiwango kikubwa katika nyanja
mbalimbali.
Kielimu, wasichana wengi
hulazimika kuacha shule mara tu baada ya kukeketwa au kuolewa, Ki-afya, ukeketaji husababisha madhara makubwa ya kiafya
yakiwemo maumivu makali, kutokwa na damu nyingi, maambukizi ya njia ya uzazi,
matatizo wakati wa kujifungua, na matatizo ya afya ya akili kutokana na msongo
wa mawazo na unyanyasaji wa kijinsia
Kiuchumi, ndoa za utotoni
huwafanya wasichana kuwa tegemezi kwa waume zao, wakikosa ujuzi, elimu au
nafasi ya kupata kipato chenye maana. Wanajikuta wakikosa uhuru wa kiuchumi na
kushindwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.
Wakati hali inaonesha matukio ya ukatili kushuka lakini zipo
changamoto ambazo wadau ambao ni mashirika yasiyo ya kiserikali katika mkoa wa
Mara wanakumbana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao.
Rhobi Samwelly mkurugenzi nishirika la Hope foe Girls and
Women in Tanzania na Nollasko Mgimba afisa ni miradi kutoka Kanisa Katoriki
Dayosisi ya Mara wanasema licha ya mafanikio yaliyopo zipo changamoto katika
jamii wanapotekeleza miradi yao.
Rhobi Samwelly anasema katika kesi za ndoa za utotoni ikiwa tayari imefika katika vyombo vya haki kwa ajili ya kutoa maamuzi lakini unakuta familia zinakwamisha kwa kufanya mazungumzo nje ya vyombo hivyo vya kutoa haki na wanakubaliana ili jambo hilo lisendelee mahakamani na kupoteza ushahidi.
Amesema pia changamoto
nyingine ni vitisho na matusi toka kwa jamii ambayo bado inashikiria mila na
desturi zilizopitwa na wakati huku akitoa wito kwa viongozi wa serikali na
kisiasa kuendelea kutoa elimu kwa jamii.
Kwa upande wake Nollasko Mgimba anasema anasema changamoto kubwa wanayipata katika jamii wakati mwingine ni kutopokelewa na jamii kutokana na baadhi yao kuona wanapinga mila zao ambazo wengine ndio vyanzo vyao vya mapato.
Amesema changamoto nyingine ipo kwenye usimamizi wa sheria na
sera zilizopo sababu jambo hili ni la kimila na viongozi wengi wanaoteuliwa au
kuchaguliwa wanatoka katika mazingira hayo hayo hivyo wanakosa nguvu kubwa ya
kuzisimamia sheria hizo kwa ajili ya kutokomeza ukatili huo sababu ni sehemu ya
mila na desturi zao lakini pia wanahofia kuhatarisha nafasi zao na kuogopa kutochaguliwa
tena na wananchi wakati wa uchaguzi.
Ametoa wito kwa wadau kushirikiana kuunganisha nguvu kwa
pamoja na wadau wa maendeleo kusaidia upatikanaji wa rasilimali katika
mapambano dhidi ya vitendo hivyo katika jamii.
SMAUJATA ni
kampeni ya kitaifa ya kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili kwa watoto nchini
Tanzania inanyofanya kazi chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii , Jinsia,
Wanawake na Makundi maalum na Joyce James ni Mwenyekiti wa SMAUJATA
Mkoa wa Mara, anasema katika mwaka huu 2025 wamepokea kesi nyingi zinazohusiana
na mimba za utotoni.
Amesema ukatili
wa kijinsia katika mkoa wa Mara umeendelea umeshamiri sana na katika mwaka wa
2025 wamepokea kesi nyingi za watoto kupewa mimba na kukatisha masomo yao na
wengine wameachishwa masomo wakiwa hawajafikia hata elimu ya sekondari wakiwa
wamepewa mimba.
“Tunayo
kampeni ya kutoa elimu mashuleni ili jamii ya mkoa wa Mara iweze kutambua
madhara ya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ndoa na mimba za utotoni, Mfano kila shule tunayoenda
kutoa elimu hasa shule za msingi tunakuta watoto wadogo ambao chini ya miaka 15
wamepewa mimba na kusitishwa masomo yao jambo ambalo linawaumiza wazazi wengi.
Tunakutana na changamoto nyingi tunazopia wakati wa kutekeleza kampeni hii mfano wazazi wengine kutotoa ushirikiano wa watukio haya lakini changamoto nyingine ni wazazi au walezi kuficha haya matukio yanayowapata watoto na sisi tunataka jamii itambue madhara ya ndoa za utotoni, Mfano wakati tunatoa elimu katika shule ya msingi Songambele iliyopo wilaya ya Musoma, walimu wameshuhudia wapo watoto ambao wamepewa mimba na kesi zao zipo katika vyombo vya sheria ili wahusika wachukuliwe hatua” Amesema Joyce James
Wanaharakati, mashirika yasiyo ya kiserikali na viongozi wa dini wamekua wakipendekeza mabadiriko ya Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hususani kwenye vifungu vya 13 na 17 vinavyoruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 na 15 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au kwa amri ya mahakama kwa madai kwamba Sheria hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na; kuruhusu mazingira fulani ya ubaguzi wa kijinsia kwa wanawake na wasichana , kuimarisha elimu na uhamasishaji wa jamii katika kukomesha tatizo la ndoa za utotoni .
Rebecca Gyumi ni Mkurugenzi wa Shirika la Msichana
Initiative, ambaye ni miongoni mwa wanaharakati nchini Tanzania, alifungua
kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kwa niaba ya watoto wote walio katika hatari
ya kuingia kwenye ndoa za utotoni dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali la
madai namba tano(5) ya mwaka 2016 kupinga uhalali wa kikatiba wa ndoa za
utotoni.
Wakati wanaharakati hao kupitia Mtandao wa Kumaliza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) wakisubiri Serikali kutekeleza hukumu hiyo, Mnamo Mei 10, 2025 Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dodoma alinukuliwa akisema baadhi ya ndoa zinagusa imani za watu.
“Baadhi ya
ndoa zinagusa maisha ya watu hivyo huwezi kubadilisha imani hizi kwa kutunga au
kurekebisha sheria bila kwanza kushauriana na kupata ridhaa ya watu hawa, na
ridhaa haiwezi kulazimishwa. Serikali imeelekezwa na mahakama, lakini kumbuka,
lazima tupate ridhaa ya watu wote hawa.” Alisema Dkt Ndumbaro
Baada ya
kauli ya Mhe. Dkt Damas Ndumbaro, Mtandao wa Kumaliza Ndoa za Utotoni Tanzania
pia ukaja na wito wa kuiomba serikali iharakishe mchakato wa kufanya
marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kama ilivyoelekezwa kwenye kesi ya
Rebeca Gyumi. Vilevile, tunatoa wito wa kufanyika kwa marekebisho ya sheria
nyingine zote zinazowanyima wasichana haki zao, ili kuimarisha ulinzi wa watoto
wa Tanzania
Wakieleza
kutambua kuwa mila na imani za kidini ni sehemu ya utambulisho wa jamii,
tunasisitiza kwa nguvu zote kuwa haki za watoto haziwezi kuwa kafara ya mila au
tafsiri za kidini ambazo zinawaweka watoto hasa wasichana katika hatari ya ndoa
za utotoni ambazo zina madhara makubwa kiafya, kielimu, kiuchumi, na
kisaikolojia.
“Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania kama wadau wa haki za watoto tumesikitishwa na kauli iliyotolewa na Waziri wa katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro siku ya tarehe 10/5/2025 wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Wakati wote kunapokua na mgangano kati ya dini,mila na sheria, sheria ndio utawala na kutumika kwa sababu sheria ndio inayoleta usawa, na dini zipo tofauti kuna wengine wakristo, wengine waislam na kuna wengine hawana dini kabisa hivyo ni vigumu kusema utashi wa dini ndio uongoze maslahi ya watu wote” Wanajukwaa la TECMN
Wakati dunia ikiadhimisha siku 16 za Uanaharakati kwa kauli mbiu madhubuti ya kupinga na kutokomeza ukatili kijinsia ukatili dhidi ya mwanamke na mottomwaka 2024 isemayo Kuelekea Miaka 30+ ya Beijing: Chagua Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia lakini bado baadhi ya maeneo nchini ikiwa ni pamoja na mkoa wa Mara yanaonekana kutotekeleza kwa vitendo kauli hiii.