Na Angela Sebastian-Bukoba,
Washitakiwa wawili mkoani Kagera wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa mashtaka mawili tofauti moja ni la baba kumbaka binti yake wa miaka 15.
Mshitakiwa Arodi Anold Mberwa (40) mkazi wa wilaya ya Bukoba amehukumiwa kwenda jela miaka 30 katika mahakama ya wilaya ya Bukoba mkoani hapa baada ya kushiriki ngono au mahusiano yaliyokatazwa kisheria na binti yake wa kumzaa wa miaka 15 ambaye alikuwa amemaliza darasa la saba.
Wakili wa Serikali Elias Subi ameeleza kuwa, mshitakiwa Arodi alikuwa haishi na mke wake alikuwa ameishaachana naye muda mrefu hivyo binti alikuwa anaishi na shanghazi yake mkoa wa Morogoro na ndiko alimalizia darasa la saba alipomaliza shule ya msingi alirudi kuishi na baba yake mzazi.
Subi ameeleza kuwa binti huyo wakati akiendelea kuishi na baba yake ndani ya mwaka mmoja siku moja mama yake alikuja kutembea pale nyumbani hivyo binti alipata kumfahamu mama yake na sehemu alipokuwa anaishi.
“Baada ya kujua mama yake anaishi sehemu fulani alitoroka nyumbani na kwenda kwa mama yake mzazi na kwa kuwa binti alikuwa ameishachoshwa na vitendo hivyo alivyokuwa akufanyiwa na baba yake alimwambia mama yake ambaye naye alitoa taarifa kituo cha polisi na taratibu za kumkamata mshtakiwa zilifanyika” amesema Subi.
Amesema Agosti 28 mwaka jana Arodi alifikishwa mahakamani na June 16, mwaka huu mahakama imemtia hatiani na kumuhukumu kwenda jela miaka 30 chini ya kifungu cha 158 kifungu kidogo cha (1) (a) na kifungu cha 159 cha sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Aidha hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi mwandamizi mahakama ya hakimu mkazi Bukoba Yona Wilson na
Mawakili upande wa serikali katika shitaka hilo walikuwa ni Elias Subi pamoja na Deocadia Kabagambire.
Wakati huohuo mahakama kuu kanda ya Bukoba imemuhukumu kwenda jela miaka 30 Baraka Jastine Daudi maarufu kama Muungula (34) mkazi wa kata ya Kaisho wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera baada ya kujaribu kumuua Jastine Felician (68) mkazi wa kata hiyo.
Mwanasheria wa serikali Judith Mwakyusa amesema kuwa, mnamo Novemba 11,2022 mshtakiwa Baraka alivamia nyumbani kwa muhanga akiwa na kitu chenye ncha kali akidai kuwa alikuwa anamdai mhanga fedha za kumfyatulia matofali.
"Baraka ambaye ni mshitakiwa alimjeruhi mhanga sehemu ya uso na kusababisha majeraha makubwa na kutokana na majeraha hayo alifanyiwa upasuaji zaidi ya mara moja na kumpandikiza nyama usoni" amesema Mwakyusa
Aidha ameeleza kuwa, baada ya mahakama kusikiliza ushahidi uliotolewa imemtia hatiani mshitakiwa na kumuhukumu kwenda jela miaka 30.
Hukumu hiyo, ilitolewa na jaji wa mahakama kuu kanda ya Bukoba Lilian Itemba huku wanasheria wa serikali wakiwa ni Matlida Assey pamoja na Agness Awino