👉Vijana wahimizwa kujiepusha na dawa za kulevya, pombe na kutumia fursa za maendeleo
Na Robinson Wangaso, Musoma
Changamoto za afya ya akili zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya vijana kutumia vibaya simu za mkononi na mitandao ya kijamii, hali inayochochea mmomonyoko wa maadili na kuathiri maendeleo yao binafsi na ya jamii.
Hayo yalisemwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Fredy Isaya Edward, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu afya ya akili katika Kongamano la Vijana (Youth Platform) lililofanyika Agosti 5, 2026, katika Ukumbi wa Shule ya Ufundi Musoma, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026.
Fredy alisema afya ya akili ni msingi muhimu wa maisha ya kila kijana, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kujifunza kukabiliana na changamoto za maisha kwa njia sahihi, kutumia teknolojia kwa uwajibikaji na kutafuta msaada wa kitaalamu wanapokabiliwa na matatizo ya kisaikolojia ili kulinda mustakabali wao.
Kongamano hilo liliwakutanisha zaidi ya vijana 1,000 kutoka kata zote za Manispaa ya Musoma, pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali, vyuo na shule za sekondari. Washiriki walipata elimu kuhusu uzalendo, uadilifu, kujitolea, fursa za kiuchumi na ajira, Sera ya Maendeleo ya Vijana, uraia na falsafa ya Mwenge wa Uhuru 2026.
Naye Chausiku Manyama, mjumbe wa Baraza la Vijana la Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, alisema matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe kupita kiasi ni miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la matatizo ya afya ya akili kwa vijana. Alieleza kuwa tabia hizo huathiri uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuwaweka vijana katika hatari ya magonjwa ya kuambukiza pamoja na changamoto za afya ya uzazi.
Aliwataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, kudhibiti mihemko na tamaa zinazozidi uwezo wao wa kiuchumi, akieleza kuwa kufanya hivyo kutawasaidia kulinda afya zao, kutimiza ndoto zao na kuwa wazazi wenye afya na malezi bora katika siku zijazo.
Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, aliwahimiza vijana kuwa waadilifu, wabunifu na kuthubutu kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ili kujijengea maisha bora. Alisema ujana ni kipindi muhimu cha kujifunza, kujenga uwezo na kuwekeza katika maendeleo ya kiuchumi, huku akisisitiza kuwa kuthubutu ndiko kunakomwezesha mtu kupiga hatua kutoka ngazi moja ya maendeleo kwenda nyingine.
Kongamano hilo lilihitimishwa kwa uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Vijana wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma. Nado Mawindo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Zabron Mgini kuwa Katibu, Ibrahimu Majura kuwa Mtunza Hazina, huku Chausiku Manyama na Fabian Aloyce wakichaguliwa kuwa wajumbe. Washiriki walieleza kuwa kongamano hilo limewapa maarifa yatakayowasaidia kulinda afya ya akili, kutumia teknolojia kwa uwajibikaji na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na Taifa



