Na Angela Sebastian, Bukoba
MATUKIO ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto mkoani Kagera yamepungua kutoka 284 mwaka 2025 hadi 250 mwaka 2026, huku ubakaji ukiendelea kuwa changamoto kubwa inayotishia usalama wa wanawake na watoto, hali iliyoibua wadau na viongozi mbalimbali kutoa wito kwa mamlaka husika kutunga sheria kali na hatua kali dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kashai, Manispaa ya Bukoba, Meya wa Manispaa hiyo, Acton Rwankomezi, amezishauri mamlaka husika kuweka sheria kali zitakazowabana wahusika, akieleza kuwa baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa lakini baadaye kuachiwa licha ya kuwepo kwa ushahidi, hali inayowaongezea waathirika maumivu ya kisaikolojia na kuwakosesha imani katika upatikanaji wa haki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii mkoani Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi Charles Mimata, alisema ubakaji, ulawiti wa watoto na mauaji ni miongoni mwa vitendo vinavyoendelea kuacha majeraha makubwa katika jamii, huku akibainisha kuwa Wilaya ya Bukoba inaongoza kwa matukio 60 yaliyoripotiwa kati ya Januari na Novemba 2026.
"Kati ya hayo, 51 ni ubakaji, sita ulawiti, mauaji ya mtoto mmoja na mauaji ya wanawake mawili na Wilaya nyingine ni Karagwe yenye matukio 48, Missenyi 38, Muleba 31 na Biharamulo 15" Mimata
Akieleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika, Mimata alisema katika kesi 54 za mauaji zilizofikishwa mahakamani kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, watuhumiwa 18 wamehukumiwa adhabu ya kifo na 36 kifungo cha maisha.
Alisema pia katika kesi 10 za ulawiti, watuhumiwa wanane wamehukumiwa kifungo cha maisha na wawili adhabu ya kifo, huku katika kesi 65 za ubakaji, watuhumiwa 16 wamehukumiwa kifungo cha maisha na 49 kifungo cha miaka 30 jela.
Aliongeza kuwa baadhi ya kesi nyingine bado ziko katika hatua mbalimbali za kisheria, zikiwemo uchunguzi na upatikanaji wa mashahidi. Katika juhudi za kuzuia vitendo hivyo, alisema Jeshi la Polisi limeendesha mikutano zaidi ya 960 kupitia wakaguzi wa kata kuanzia Januari hadi Novemba 2026, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na kuripoti ukatili.
Aidha, Dawati la Jinsia na Watoto limeimarishwa pamoja na huduma ya kupokea taarifa kupitia namba 0699 913 200 inayopatikana saa 24 bila malipo.
Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, ubakaji umepungua kutoka matukio 221 mwaka 2025 hadi 205 mwaka 2026, wakati ulawiti umeongezeka kutoka 12 hadi 16 na mauaji ya watoto kutoka tisa hadi 10.
"Hata hivyo, mauaji ya wanawake yamepungua kutoka matukio 42 hadi 19 katika kipindi hicho, hali inayoonesha kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna haja ya kuongeza nguvu katika kupambana na aina zote za ukatili"alisema
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Proscovia Jakamwambi, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza ulinzi kwa wanawake na watoto, huku akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji ushirikiano wa familia, serikali na wadau mbalimbali.
Alisema vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa jamii, vinaongeza umaskini na kuchochea chuki na visasi, hivyo wananchi hawapaswi kufumbia macho matukio yanayotokea katika familia zao.
Alisisitiza kuwa kampeni ya siku 16 inalenga kuhamasisha jamii kutambua, kuzuia na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili, akiwataka wananchi kuwafichua wote wanaojihusisha na ubakaji na ulawiti bila kujali uhusiano wao wa kifamilia. Alisema kulinda wanawake na watoto si jukumu la Jeshi la Polisi pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha jamii inakuwa salama, yenye haki na isiyovumilia ukatili wa kijinsia.










Maoni ()