Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema
matumizi ya Sayansi ya Kijiografia na Akili Unde (Artificial Intelligence)
katika kutafuta, kukusanya na kuchambua takwimu za kijiografia yatasaidia
kuboresha shughuli za upimaji wa ardhi nchini, kuongeza ufanisi na kuchochea
ubunifu unaoendana na maendeleo ya teknolojia duniani.
Mhe. Mmuya
amesema hayo jijini Mwanza, wakati akifungua Kongamano la Wapima Ardhi Tanzania
pamoja na Mkutano Mkuu wa 30 wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Ardhi Tanzania
(IST), akieleza kuwa matumizi ya teknolojia hizo ni muhimu katika kuimarisha
mifumo ya upimaji na usimamizi wa ardhi ili kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo.
Amesema
kauli mbiu ya kongamano hilo inaakisi utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na
mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayohitaji matumizi ya
sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya sekta mbalimbali
nchini.
Aidha,
amesisitiza umuhimu wa Wapima Ardhi kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa
kutumia maarifa na mifumo ya kisasa katika kutafuta na kuchakata taarifa za
kijiografia zitakazosaidia kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za upimaji na
usimamizi wa ardhi.
Kongamano
la mwaka huu limeongozwa na kauli mbiu isemayo: “Sayansi ya Kijiografia, Akili
Unde na Upimaji Ardhi wa Kisasa: Kuchochea Ubunifu kwa ajili ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo ya 2050.”

Maoni ()